SPORTS ACADEMY KUJENGWA KAHAMA

 Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) Wallace Karia, akizungumza katika mkutano na wadau wa Michezo wilayani Kahama mkoa wa Shinyanga.

Na Mwandishi Wetu,

Shinyanga. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeridhia kujengwa kwa kituo cha kukuza vipaji vya mpira wa miguu wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, katika eneo maalumu la uwekezaji la Buzwagi (BSEZ), lililokuwa mgodi wa uchimbaji wa dhahabu wa Barrick Buzwagi. 

Kituo hicho kitakuwa na uwezo wa kubeba watoto zaidi ya 200 kwa wakati mmoja, kikilenga kuibua na kukuza vipaji vya vijana hususan kutoka kanda ya ziwa, huku kikiwa cha tatu nchini baada ya vile vya Kigamboni jijini Dar es Salaam na Mnyanjani mkoani Tanga. 

Akizungumza leo Jumatano Februari 25, 2026 Rais wa TFF, Wallace Karia, ameidhinisha ujenzi huo wakati akizungumza na wadau wa michezo wilayani Kahama, huku akielekeza uongozi wa soka wa mkoa kwa kushirikiana na wilaya kuandaa mpango wa utekelezaji wa mradi huo kwa haraka ili kuanza maboresho mapema iwezekanavyo, 

“Hili jambo wala si la kuomba, nielekeze uongozi wa soka mkoa, shirikianeni na wilaya muandae mpango wa makubaliano ya utekelezaji wa jambo hili haraka, ikiwezekana Machi Mosi, 2026 tuanze maboresho” amesema Karia.

Aidha, ameahidi kuwa hatua za awali za maandalizi zitaanza mara moja kwa kuandaa taarifa muhimu zitakazowezesha ujenzi wa kituo hicho kukamilika ndani ya muda mfupi. 

Naye Ofisa Michezo wa Manispaa ya Kahama, Mwaita Mwinyimkuu amesema eneo la BSEZ lina miundombinu inayoweza kutumika mara moja kwa shughuli za kituo hicho, 

Ametaja miundombinu hiyo kuwa ni pamoja na, “Uwanja mkubwa wa mpira wa miguu (mita 132 kwa 66 mita za mraba 8,712), viwanja vya netiboli na mpira wa wavu, ukumbi wa mazoezi ya ndani (Gym), nyumba 40 zenye uwezo wa kuchukua watu zaidi ya 200, mabweni yanayoweza kuhudumia zaidi ya vijana 300 kwa wakati mmoja, ofisi za utawala, madarasa na kumbi ndogo za mikutano pamoja na miundombinu ya vyoo na mabafu”

Baadhi ya wadau wa michezo wilayani Kahama, akiwemo Edwin Soko, wameiomba TFF kuharakisha ukarabati wa majengo yaliyopo ili kituo kianze kupokea vijana mapema,

“Mimi ninachoomba TFF waharakishe ukamilishaji wa kituo hiki, majengo yapo, yarekebishwe kianze kupokea watoto na sisi kanda hii tuzalishe wanamichezo wakubwa” amesema. 

Uamuzi huo wa TFF unakuja siku mbili kabla ya mkutano mkuu wa TFF unaotarajiwa kufanyika wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, ukitarajiwa kukutanisha zaidi ya wadau 600 wa michezo kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Kwa mujibu wa Karia, TFF imevutiwa na sifa za eneo la Buzwagi, likielezwa kuwa na uwezo wa kuwa kitovu muhimu cha kuibua na kukuza vipaji vya vijana na kuinua kiwango cha mpira wa miguu nchini.


Chapisha Maoni

0 Maoni