Miradi hiyo inayotekelezwa na kampuni kubwa za ndani na nje ya nchi inatakiwa kukatiwa bima hivyo kuongeza wigo wa mapato kwa shirika la bima Zanzibar
Na Mwandishi Wetu,
Unguja. Wakati kukiwa na miradi mikubwa inayotekelezwa na kampuni kubwa za ndani na nje ya nchi, serikali imelitaka Shirika la Bima la Zanzibar (ZIC) kutumia fursa hiyo kuongeza mchango wake wa gawio kwa serikali.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Fedha na Mipango Dk Maliki Juma Akil ambapo amesema licha ya jitihada zinazoendelea lakini bado kuna fursa kubwa katika miradi mikubwa inayotekelezwa Zanzibar.
"Serikali inataka fedha na fedha itazipata kupitia mashirika kama haya, ZIC hii ni fursa kwenu kuhakikisha mnawakatia bima kampuni zinazojenga miradi na jambo ambalo litasaidia kuongeza Galion kwa serikali," amesema Dk Malik
Waziri huyo ametoa kauli hiyo Machi 8, 2026 wakati wa futari iliyoandaliwa na ZIC kwa ajili ya kuongeza mshikamano na upendo kwa wateja wake.
Amesema shirika hilo ni miongoni mwa mashirika makongwe ambayo yametoka mbali na kuasisiwa miaka mingi na yamekuuwa imara pamoja na kupitia misukosuko mbalimbali.
Kama taasisi hususan ya kifedha misukosuko ndio mahali pake inapanda na kushuka lakini hatimaye tumekuwa na shirika ambalo linajitegemea na linatoa mchango wake kwa serikali.
Amesema biashara ya Bima imeendelea kuwa biashara nzuri katika kuendesha nchi yoyote lakini inakuwa muhimu zaidi kwa nchi ambayo inakuwa na shughuli nyingi za kiuchumi na inakua kama nchi inavyokuwa.
"Nchi yetu ina miradi mingi na miradi hiyo ambayo inatumia fedha nyingi iwe fedha za mfadhili zinazokuja kama mkopo au fedha za ndani," amesema
Mkurugenzi Shirika la Bima Zanzibar Jape Ussi Khamis tayari wameanza kukata bima kwenye kampuni hizo hivyo wataongeza jitihada kuhakikisha wanazifikia nyingi zaidi.
"Japo sio zote lakini zipo ambazo tumeanza kuzikatia bima, jambo la kuzingatia ni kuongeza wigo katika bima," amesema
Amesema sekta ya bima ina jukumu muhimu katika kulinda mali na uwekezaji kwa wananchi na taasisi mbalimbali dhidi ya hatari zisizotarajiwa.
"Kupitia huduma za sekta hiyo zinasaidia kuongeza uthabiti wa kifedha kwa wananchi biashara na serikali na kuchangia maendeleo endelevu ya nchi," amesema
Hata hivyo alisema kwa upande wa shirika hilo wanaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha taasisi yao ambapo hatua hizo ni pamoja na kuimarisha huduma kwa wateja, kuimarisha usimamizi wa hatari kuendeleza bidhaa mpya pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji latika uendeshaji wa shughuli zake.
Mwisho.


0 Maoni