Na Mwandishi Wetu
Shinyanga. Kamati ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga imelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga chini ya uongozi wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, kwa juhudi zake za kudhibiti vitendo vya uhalifu na kuimarisha hali ya usalama pamoja na amani kwa wananchi.
Pongezi hizo zimetolewa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maridhiano, Amani, Mila na Desturi Mkoa wa Shinyanga, Shehe Balilusa Khamis, alipokuwa akizungumza kwa niaba ya kamati hiyo. Katika tukio hilo, alikuwa ameambatana na viongozi mbalimbali wa dini, wazee wa kimila pamoja na Mkuu wa Machifu wa Mkoa wa Shinyanga.
Shehe Khamis amesema juhudi zinazofanywa na Jeshi la Polisi katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu zimechangia kurejesha utulivu na kuimarisha hali ya amani katika jamii.
Aidha, ametoa wito kwa wananchi kupuuza taarifa zisizo za kweli zinazoweza kuleta hofu au taharuki, na badala yake kushirikiana na vyombo vya dola kwa kutoa taarifa sahihi zitakazosaidia kukabiliana na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.
Ameongeza kuwa umoja na mshikamano kati ya viongozi wa dini, viongozi wa kimila pamoja na vyombo vya usalama ni nguzo muhimu katika kudumisha amani, utulivu na maendeleo ya jamii.
Kwa upande wake, Mtemi Kidola wa II, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Machifu Mkoa wa Shinyanga, ametoa wito kwa wazee na viongozi wa jamii kuendelea kuwakumbusha vijana kuzingatia maadili mema, kuheshimu sheria za nchi na kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama wa jamii.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Janeth Magomi, ameishukuru Kamati ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga kwa pongezi hizo pamoja na ushirikiano wanaoendelea kuutoa katika kuimarisha hali ya usalama na amani ndani ya jamii.
SACP Magomi ameiomba kamati hiyo kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa kutoa elimu kwa jamii, kuhimiza utoaji wa taarifa sahihi kwa vyombo vya usalama pamoja na kuendelea kuwa sehemu ya juhudi za kudumisha amani, utulivu na usalama wa wananchi.
Mwisho.

.jpeg)


0 Maoni