Na
Mwandishi Wetu, Shinyanga.
Kishapu. Miradi 45 ya maendeleo yenye thamani
ya Sh18 bilioni inatarajiwa kuzinduliwa katika Mkoa wa Shinyanga wakati wa mbio
za Mwenge wa Uhuru mwaka 2026.
Miradi hiyo inatekelezwa katika wilaya za
Kishapu, Shinyanga na Kahama, huku ikilenga kuboresha huduma na kuongeza fursa
za maendeleo kwa wananchi.
Akizungumza leo, Agosti 18, 2026 wakati wa
mapokezi ya Mwenge wa Uhuru katika kijiji cha Mwigumbi, kata ya Mondo
Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mboni Mhita,
amesema miradi hiyo itawanufaisha wananchi moja kwa moja.
“Kwa Mkoa wa Shinyanga wenye wilaya tatu,
Mwenge wa Uhuru utakwenda kuzindua miradi 45 ambayo itagharimu Sh18 bilioni.
Miradi hii itakwenda kunufaisha wananchi moja kwa moja,” amesema Mhita.
CRDB yawataka wananchi kuwa makini
katika uwekezaji
Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa
Benki ya Ushirika na Maendeleo Vijijini (CRDB), Mkurugenzi wa Mikopo wa benki
hiyo, Exavery Makwi, amewataka wananchi kutulia na kufanya maamuzi sahihi kabla
ya kuwekeza fedha zao katika biashara.
Makwi amesema baadhi ya wananchi wamekuwa
wakigawanya fedha zao katika biashara nyingi bila kuwa na mpango mzuri, jambo
ambalo linaweza kusababisha kushindwa kufuatilia matumizi na hatimaye kupoteza
fedha.
“Wananchi tulizeni akili kabla ya kuwekeza
katika biashara. Usije ukajikuta unawekeza pesa zako katika biashara nyingi,
matokeo yake zinaishia pasipo kujulikana. Lakini ukituliza akili na pesa zako
zikiwa benki, una nafasi ya kuwekeza katika biashara sahihi,” amesema.
Tawi la CRDB Maganzo lagharimu Sh700
milioni
Makwi amesema ujenzi wa jengo la tawi la CRDB
Maganzo umegharimu Sh700 milioni na kwa sasa tawi hilo lina wafanyakazi wanane.
Amesema pamoja na huduma mbalimbali za
kifedha, benki hiyo imeendelea kuboresha huduma zake kwa kutoa mikopo isiyo na
riba pamoja na kuwezesha wananchi kupata vifaa vya kisasa vya kilimo.
“Ujenzi wa jengo la tawi hili la Maganzo
umegharimu kiasi cha Sh700 milioni na kwa sasa tuna wafanyakazi wanane. Pamoja
na huduma zote za kifedha tunazotoa, pia tumeboresha huduma kwa kutoa mikopo
isiyo na riba,” amesema Makwi.
Ameongeza kuwa CRDB pia inakopesha vifaa vya
kilimo cha kisasa, ikiwemo matrekta, plau na vifaa vingine vinavyoweza
kuwawezesha wakulima kuongeza tija katika uzalishaji.
Mwang’ora aipongeza CRDB kwa mikopo
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa,
Wazo Michael Mwang’ora, amepongeza CRDB kwa kutoa mikopo kwa wananchi, hususan
wafanyabiashara, pamoja na kuwawezesha wakulima kupata vifaa vya kisasa vya
kilimo.
Mwang’ora amewataka wananchi wanaopata mikopo
kuhakikisha wanaitumia kwa shughuli zenye tija ili waweze kurejesha kwa wakati.
“Unapochukua mkopo, nenda kafanye kazi na urejeshe kidogo kidogo. Nitoe pongezi kwa kutoa mikopo, mingine ikiwa isiyo na riba, sambamba na vifaa vya kilimo cha kisasa ambavyo vinawezesha wakulima kuwa na kilimo chenye tija,” amesema.
Serikali yapewa pongezi
Mwang’ora pia ameipongeza Serikali kwa kuweka
mazingira yanayowawezesha wawekezaji kuwekeza nchini, akisema uwekezaji huo ni
chachu ya maendeleo kwa wananchi.
“Tunatoa pongezi na shukrani kwa Serikali kwa
kuwawezesha wawekezaji kuwekeza katika nchi yetu. Hii ni chachu ya maendeleo
kwa wananchi,” amesema.
Picha




.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
.jpeg)
0 Maoni