Mkuu wa Takukuru mkoa wa Shinyanga Donasian Kessy akizungumza na vyombo vya habari wakati wa kutoa taarifa ya robo ya pili ya mwaka kuanzia Oktoba hadi Desemba, 2025.
Shinyanga. Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Donasian Kessy, ametangaza kuwa taasisi hiyo imefanikiwa kuokoa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Sh. 51,752,600 katika kipindi cha robo ya pili (Oktoba–Desemba 2025), vifaa hivyo vilinunuliwa na mzabuni kwa ajili ya mradi wa ujenzi wa nyumba za watumishi wa Shule ya Msingi Magongwa, lakini havikuwasilishwa kwenye mradi huo.
Akizungumza Machi 4, 2026 katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika katika Ofisi za Takukuru, Manispaa ya Shinyanga, Kessy alisema kuwa baada ya ufuatiliaji wa karibu, taasisi hiyo ilimtaka mzabuni (jina limehifadhiwa) kuwasilisha vifaa hivyo mara moja kwenye mradi husika uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Msalala.
Kwa mujibu wa Kessy, vifaa vilivyookolewa ni pamoja na nondo, vigae (25x40), vifaa vya umeme, vifaa vya maji, vyoo, gypsum board na rangi. Alieleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za Takukuru kuhakikisha fedha za umma na rasilimali za miradi ya maendeleo zinalindwa na kutumika kama ilivyokusudiwa.
Mbali na hilo, Kessy alisema elimu ya kupambana na rushwa inayotolewa na Takukuru imeanza kuzaa matunda katika Halmashauri ya Ushetu, alibainisha kuwa mapato ya idara ya afya yameongezeka kwa asilimia 366 kwa mwezi, kutoka wastani wa Sh. milioni 3 hadi Sh. milioni 14, Ongezeko hilo limechangia kuboresha huduma za afya kwa wananchi na kupunguza malalamiko ya awali kuhusu upotevu wa mapato.
Katika kipindi hicho cha robo ya pili, Takukuru ilipokea jumla ya malalamiko 39, kati ya hayo 22 yanahusu tuhuma za rushwa na yapo katika hatua mbalimbali za uchunguzi, huku malalamiko 17 yasiyohusu rushwa yakielekezwa kwenye idara zinazohusika kwa hatua zaidi.
Kwa robo ya tatu (Januari hadi Machi 2026), Takukuru imeweka mikakati kadhaa ya kuimarisha mapambano dhidi ya rushwa, mikakati hiyo ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa umma, kufanya uchambuzi wa mifumo ya utendaji katika taasisi za umma na binafsi, kufuatilia matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo, pamoja na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wa mkoa.
Kessy alihitimisha kwa kutoa wito kwa wananchi kushirikiana kikamilifu na Takukuru kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kupitia namba ya bure 113, akisisitiza kuwa ushirikiano wa jamii ni nguzo muhimu katika kuhakikisha uwajibikaji na maendeleo endelevu.


.jpeg)
0 Maoni