Na Mwandishi Wetu, Geita
Geita. Mkazi wa mtaa wa Nyantorotoro B, kata ya Nyankumbu Manispaa ya Geita Catherine Kachwele, amelazimika kumtelekeza mbuzi wake kwa zaidi ya miezi miwili, kwa balozi wa shina namba 20 katika mtaa huo, baada ya kubaini kuwa na jinsia mbili akilitaja kuwa tukio la kwanza na la ajabu kuwahi kushuhudia katika maisha yake.
Akizungumza leo April 04, 2026 Catherine ambaye ni mtalamu wa tiba asili anabainisha miezi kadhaa iliyopita aliitwa kwenda mkoani Kigoma kutoa huduma ya matibabu, baada ya kukamilisha kazi yake mteja alimweleza kuwa na fedha pungufu ya kulipia matibabu aliyokuwa ameyatoa, hivyo kukubaliana apatiwe Mbuzi huyo kama zawadi ili kukamilisha gharama za matibabu na shukrani kwa kumponya.
Anadai aliondoka Kigoma nyakati za saa 9 usiku, hakumkagua mbuzi huyo, baada ya kuwasili nyumbani mkoani Geita, alishangazwa na kundi kubwa la watoto na majirani kumshangaa mbuzi wake ndipo alipoamua kukagua zawadi aliyopewa na kubaini kuwa alikuwa na jinsia mbili ya kike na kiume.
“Nilivyomuona akiwa katika hali hiyo nikatafuta ushauri kwa baadhi ya watu,wakaniambia muache tu,eti kuna mbuzi wengine wanaitwa shoga,wakati mwingine wanazaa hata huyu wanasema aliwahi kuzaa ila kitoto kikafa"
Aidha baada ya kuibuka kwa taharuki hiyo, Carherine alichukua uamuzi wa kumtafuta mteja wake aliyemtibu huko Kigoma, hata hivyo hakumpata kwenye simu, baadaye aliamua kumtafuta jirani yake aliyemuunganisha na mteja huyo na kufanikiwa kuwapata kwa njia ya simu ambapo, walimweleza kuwa mbuzi huyo hakuwa wa maajabu bali alizaliwa hivyo.
Balozi shina namba 20 Nyantorotoro B, Damian Mosha alidai kupigiwa simu akiwa safarini majira ya saa tano usiku, akielezwa kuwa kulikuwa na mbuzi amefungwa porini, kutokana na dhamana aliyonayo ya uongozi, aliamuru mbuzi huyo kupelekwa nyumbani kwake wakati taratibu za kumtafuta mmiliki zikiendelea
Siku iliyofuata baada ya kurejea,wakati akimchunguza aligundua kuwa ana jinsia mbili ndipo alipoanza taratibu za kumtafuta mmiliki na kubaini alikuwa wa Catherine Kachwele,hata hivyo aligoma kuondoka naye na kutaka balozi huyo kumwachia au aendelee kukaa naye.
“Alisema ngoja niende,nikishafika nyumbani nitatuma vijana waje wamchukue,sasa katika kwenda kule ikawa jumla,baada ya kumpigia simu mama mbona hauijii mbuzi wako? Akajibu balozi mtumishi wa Mungu umuombee tu abadilike awe mbuzi wa kawaida “
Mosha ameeleza tukio hilo ni la kwanza kutokea katika mtaa huo ambapo ametoa wito kwa jamii kuachana na imani za kishirikina,akigusia namna ambavyo hata kwa wanadamu imekuwa ikitokea kwa mtu kuzaliwa na jinsia mbili.
Daktari wa mifugo Halmashauri ya Manispaa ya Geita, Jackson Mutayaba amelitaja tukio hilo kuwa la kawaida kutokea kwa wanyama ikifahamika kama, Congenital anomally kwa baadhi ya viungo kwenda katika sehemu ambayo inakuwa haikulengwa.
Pia Dk Mutayaba amesema kutokana na baadhi ya wafugaji kukosa uelewa wa kutosha kuhusu masuala ya uzazi na ukoo katika mifugo,wamekuwa wakiacha kaka na dada au mama na mtoto kuzaliana hali inayoweza kuchochea kutokea kwa mifugo kama hiyo.
Aidha Dk Mutayaba amesema ziko sababu mbalimbali zinazopelekea hali hiyo ikiwa ni pamoja na wanyama wa ukoo mmoja kuendelea kuzaliana, ambapo ameshauri wafugaji kuwa na utaratibu wa kutafuta madume katika jamii ukoo mwingine wa mifugo ikiwa ni pamoja na kuwahasi au kuwauza.Aidha ili kudhibiti hali hiyo kuendelea katika mifugo,wafugaji wameshauriwa kutoruhusu mfugo mwenye jinsia mbili kuzaa na badala yake atumike kama kitoweo.
“Inabidi ubadilishe ulete dume tofauti na ukoo ule ili kuondokana na hiyo hali ya kuzaliana na siyo mbuzi tu,hata kwenye ng’ombe yanajitokeza,kwenye nguruwe mara nyingi sana,kwahiyo hawa waliozaliwa inabidi wahasiwe ili wasiendelee kupanda dada zao au mama zao.”
Naye Sijaona Kagosha mkazi wa Nyantorotoro B, amesema kwa muda mrefu alikuwa akisikia habari za kuwepo kwa mbuzi wenye jinsia mbili lakini akaiomba Serikali kupitia watalamu wa mifugo,kutoa elimu ya kina ili kuondoa taharuki kama iliyowapata.


0 Maoni