WATOTO WANNE WAPOTEZA MAISHA BAADA YA KUANGUKIWA UKUTA WA HOSTEL, BUKOBA

Na Mwandishi Wetu, Kagera.

Bukoba. Watoto wanne wa familia mbili tofauti wamefariki dunia baada ya kuangukiwa na ukuta wa hoteli ulioporomoka kufuatia mvua kubwa iliyonyesha alfajiri katika mtaa wa Anyama, kata ya Kibeta Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera.

Tukio hilo limetokea Aprili 17, 2026 saa 11:00 alfajiri, wakati watoto hao wakiwa wamelala majumbani mwao.

Inadaiwa kuwa ukuta wa Hoteli ya Pafect ulianguka ghafla na kuangukia nyumba walizokuwa wamelala, na kusababisha vifo vyao papo hapo.

Kaimu Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa Bukoba ya Mkoa wa Kagera, Dk Charles Kaigi, amesema wamepokea miili ya watoto hao wanne, watatu wakiwa wa kike na mmoja wa kiume.

Amesema waliofariki kutoka familia ya Mikdadi Ally ni Maniath Mikdadi (4) na Nunihan Mikdadi (10), huku kutoka familia ya Edimond Matungwa waliofariki ni Elizabeth Edimond (12) na Edwin Edimond (10).

Dk Kaigi amesema uchunguzi umeonyesha kuwa watoto hao walifariki kutokana na kukosa hewa baada ya kufunikwa na kifusi kilichowajaza mchanga puani na mdomoni.

Naye, Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoani Kagera, Joseph Ngonyani amesema walipokea taarifa za tukio hilo na walipofika eneo la tukio walikuta wananchi wakiendelea na juhudi za uokoaji.

Amesema jeshi hilo lilishirikiana na wananchi kuondoa kifusi na kufanikisha kutoa miili ya watoto hao, ambayo baadaye ilipelekwa hospitali.

Aidha, amewataka wananchi kuchukua tahadhari zaidi katika kipindi hiki cha mvua kubwa kwa kuhakikisha majengo yao yanakuwa imara ili kuepusha madhara kama hayo.

Mashuhuda wamesema ajali hiyo ilitokea wakati mvua ikiendelea kunyesha, hali iliyosababisha ukuta huo kuporomoka na kuangukia nyumba mbili za jirani.

Mmoja wa mashuhuda, Anitha Jacob amesema alisikia kelele za kuomba msaada kutoka kwa majirani mapema alfajiri na alipofika eneo la tukio alikuta kifusi cha ukuta wa hoteli kimeangukia nyumba hizo huku wananchi wakijitahidi kukiondoa.

MWISHO.


TANGAZA NASI KUPITIA MAGAZETI:

 MATANGAZO YA KUPOTELEWA NA HATI YA KIWANJA, VYETI, LESENI NA MENGINE YOTE.


PIGA SIMU NAMBA: 0763955413

Chapisha Maoni

0 Maoni