Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam.
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari siku
tatu, kuhusu uwezekeno wa mvua kubwa zitzkazoweka kusababisha mafuriko, katika
baadhi ya mikoa ya Pwani ikiwemo Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na TMA leo Jumanne Aprili
07, 2026 imesema mvua hizo zinatarajia kuanza Jumatano hadi Ijumaa, zikihusisha
mikoa ya Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani, Dar es Salaam sambamba na visiwa vya
Unguja na Pemba.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa, uwezekeno wa kunyesha kwa mvua
hizo pamoja na athari zake umeainishwa kuwa wa kiwango cha kati, lakini
wananchi wametakiwa kuchukua tahadhari zote muhimu.
“Kuanzia kesho hadi Ijumaa mvua zinatarajiwa kunyesha katika
maeneo tajwa, uwezekeno wa athari zake zipo katika kiwango cha kati” Imeeleza
sehemu ya taarifa hiyo.
Hata hivyo TMA imeonya kuwa, mvua hizo zinaweza kusababisha
mafuriko katika baadhi ya maeneo na kuathiri katika shughuli za kijamii na
kiuchumi.
Wananchi wanaoishi katika maeneo ya Pwani na visiwani,
wametakiwa kuwa waangalifu zaidi kutokana na uwezekano wa ongezeko la kiwango
cha mvua.
“Umma unashauriwa kufuatilia taarifa rasmi za hali ya hewa na
kuchukua tahadhari stahiki” Imeongeza taarifa hiyo.
TMA imeongeza itaendelea kufuatilia mwenendo wa hali ya hewa
na kutoa taarifa zaidi kadri itakavyo hitajika.


0 Maoni