Na Mwandishi Wetu, Iringa.
Katika kijiji cha
Kalenga, mkoani Iringa, yapo Makumbusho ya Mkwawa mahali palipojaa historia
nzito ya upinzani dhidi ya ukoloni, Makumbusho haya yanahifadhi kumbukumbu za
shujaa wa kabila la Wahehe, Chifu Mkwawa, aliyepambana kwa ujasiri mkubwa dhidi
ya Wajerumani mwishoni mwa karne ya 19.
Umaarufu wake uliongezeka zaidi baada ya ushindi mkubwa dhidi ya Wajerumani katika Vita ya Lugalo mwaka 1891, baada ya ushindi huo Wajerumani walipanga kulipiza kisasi kwa nguvu kubwa zaidi, Mwaka 1894 walivamia ngome ya Kalenga kwa silaha za kisasa na kulazimisha Wahehe kukimbia.
Hata hivyo, Mkwawa
hakukamatwa alianza vita vya msituni (guerrilla warfare), akijificha na
kuendelea kushambulia maadui zake kwa kushtukiza.
Kwa miaka kadhaa, Mkwawa aliendelea kuwasumbua Wajerumani, akibadilisha maeneo ya kujificha na kutumia mbinu za vita za kuvizia, lakini kadiri muda ulivyopita, nguvu zake zilianza kupungua kutokana na uhaba wa rasilimali na usaliti kutoka kwa baadhi ya watu waliokuwa karibu naye, Wajerumani waliweka msako mkali wakimtafuta kila kona.
Mwaka 1898, baada ya kuzingirwa na askari wa Kijerumani katika eneo la msitu karibu na Kalenga, ilibainika kuwa hakuwa na njia ya kutoroka, akiwa amechoka vita na akiona hatari ya kukamatwa hai, Mkwawa alichukua uamuzi mgumu alijiua kwa kujipiga risasi, akiepuka kudhalilishwa na maadui zake.
Baada ya kifo chake, Wajerumani walikata kichwa chake na kukipeleka Ujerumani kama ishara ya ushindi, Hata hivyo baada ya utawala wa Mjerumani alikuja Muingereza ndio wahehe walipoomba warudishiwe fuvu la kiongozi wao, na baada ya Tanzania kupata uhuru, juhudi zilifanyika kurejesha fuvu hilo nyumbani.
Mwaka 1954, fuvu la Mkwawa lilirejeshwa nchini na sasa linahifadhiwa katika Makumbusho ya Kalenga kama alama ya heshima na kumbukumbu ya shujaa huyo.
Makumbusho ya Mkwawa si tu sehemu ya kihistoria, bali pia ni ishara ya uzalendo na mapambano ya Waafrika dhidi ya ukoloni, wageni wanaotembelea eneo hilo hupata fursa ya kujifunza historia ya kweli ya upinzani na kujivunia urithi wa mashujaa wa Tanzania.
Kwa ujumla, simulizi ya
Mkwawa ni hadithi ya ujasiri, mapambano, na kujitolea kwa ajili ya uhuru, makumbusho
yake yanaendelea kusimulia historia hiyo kwa vizazi vya sasa na vijavyo,
yakikumbusha kuwa uhuru uliopatikana ulilipiwa kwa gharama kubwa.




0 Maoni