KLINIKI MPYA YAFUNGUA MLANGO WA MATUMAINI, WAATHIRIKA WA DAWA ZA KULEVYA

Na Mwandishi Wetu, Shinyanga.

Shinyanga. Kuna simulizi nzito inayozidi kujitokeza, simulizi ya vijana wanaoangamia kimya kimya kutokana na matumizi ya dawa zenye asili ya kulevya, wakati ambapo wengi walidhani tatizo kubwa ni heroin na cocaine, ukweli mpya unaibuka kuna hatari nyingine kubwa zaidi inayochipuka kwa kasi.

Akizungumza Machi 22, 2026, Aretas Lyimo, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Tanzania, ametoa onyo kali kwa vijana, alisema wazi kuwa baadhi ya dawa tiba zinazotumika kimatibabu sasa zinageuzwa na kutumiwa kama mbadala wa dawa hatari kama heroinlakini athari zake ni mbaya zaidi.

Kwa mujibu wa Lyimo, dawa hizi si tu zinaharibu afya, bali pia zinaweza kusababisha vifo kwa haraka, mbaya zaidi mtu anaweza kutumia kati ya miaka 10 hadi 20 kupona ikiwa ataweza kupona kabisa.

Wakati huo huo, matumizi ya Sikanka (bangi iliyosindikwa) yamekuwa yakiongezeka, dawa hii imehusishwa moja kwa moja na kuongezeka kwa wagonjwa wa afya ya akili, jambo linalotia hofu kubwa kwa jamii.

Katika hatua ya kupambana na janga hili, jengo jipya la kliniki ya uraibu wa dawa za kulevya limezinduliwa katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga. Kliniki hii inaleta matumaini mapya kwa waathirika wengi waliokuwa wakilazimika kusafiri hadi Mwanza kupata matibabu.

Kwa mujibu wa Redempta Mbatia kutoka THPS, lengo kuu ni kupunguza gharama na kuwafikia vijana wengi zaidi wanaohitaji msaada wa haraka.

Ujenzi wa kliniki hii umewezeshwa na CRDB Bank, ambao walitoa Shilingi milioni 140. Meneja wa kanda ya Magharibi, Jumanne Wagana, alisema huu ni sehemu ya kurudisha kwa jamii na wataendelea kusaidia sekta ya afya.

Kwa Ibrahim Selfu alieleza kuwa safari haikuwa rahisi, akiwa mraibu kwa zaidi ya miaka 10, alipoteza kazi yake kama ajenti wa magari na hata kutengwa na familia yake.

“Nilipitia wakati mgumu sana, lakini sasa nimepona. Naamini wengine wanaweza pia,” anasema kwa matumaini.

Mbali na afya, matumizi ya dawa hizi yanaongeza uhalifu, maambukizi ya magonjwa kama VVU/UKIMWI, changamoto za afya ya akili pamoja na vifo visivyotarajiwa.

Huduma za MAT (Medication Assisted Treatment) zimeonekana kuwa suluhisho muhimu katika kupunguza madhara haya, lakini mapambano bado ni makubwa.

Chapisha Maoni

0 Maoni