Mbunge wa jimbo la Shinyanga mjini ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Patrobas Katambi akizungumza na Mkandarasi wa miradi ya baarabara ya kelekea Hospital ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga (Mwawaza) na Stendi ya mabasi, Edwin Rwezahura, katika eneo la ujenzi wa Stendi kuhusiana na maendeleo ya miradi hiyo. Picha na Mwandishi Wetu.
Mbunge wa Shinyanga Mjini na Waziri wa Mambo ya Ndani, Patrobas Katambi, amemtaka mkandarasi wa miradi ya barabara ya Mwawaza na stendi ya mabasi ya mkoa kufanya kazi usiku na mchana ili kukamilisha miradi hiyo kwa wakati, akisisitiza kuwa hakuna muda wa nyongeza utakaotolewa nje ya makubaliano ya mkataba.
Na Mwandishi Wetu, Shinyanga
Akizungumza Februari 23, 2026 baada
ya kukagua maendeleo ya barabara inayoelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa
Shinyanga (Mwawaza) pamoja na stendi ya mabasi iliyopo Kata ya Kizumbi,
Manispaa ya Shinyanga, Katambi alisema hajaridhishwa na kasi ya utekelezaji wa
mradi huo licha ya mkandarasi kupewa malipo ya awali ya Sh. 3.9 bilioni.
“Hali inayoonekana hapa hairidhishi
kabisa. Nilitegemea utekelezaji uwe umefikia thamani ya fedha mliotanguliziwa.
Mkandarasi unatakiwa kufanya kazi usiku na mchana kukamilisha kazi kwa muda
uliowekwa katika mkataba; hakuna muda utakaoongezwa. Tuko tayari kuvunja
mkataba kama mambo hayaeleweki,” alisema Katambi.
Kwa upande wake, mkandarasi wa
miradi hiyo, Edwin Rwezahura,
alisema wako tayari kuongeza kasi ya kazi ili kuhakikisha miradi yote inakamilika
kwa muda uliopangwa.
“Tuko tayari kufanya kazi usiku na
mchana katika miradi yote miwili ili kumaliza ndani ya muda ulioandikwa katika
mkataba,” alisema Rwezahura.
Historia ya Mgogoro
Mkataba wa ujenzi wa barabara ya
Mwawaza na stendi ya mabasi ulisainiwa Julai 2025, ukishuhudiwa na Kamati ya
Ulinzi na Usalama ya Mkoa wa Shinyanga.
Januari 9, 2026, Mkuu wa Mkoa wa
Shinyanga, Mboni Mhita, alikagua
mradi huo na kueleza kutoridhishwa na maendeleo yake, akimtaka mkandarasi
kuongeza kasi ya utekelezaji. Inadaiwa kuwa baada ya ukaguzi huo mkandarasi
aliondoa vifaa katika eneo la mradi.
Mnamo Januari 29, 2026, Mkuu wa
Wilaya ya Shinyanga alikagua tena utekelezaji wa maagizo hayo na kukuta hali
ikiwa haijabadilika, hatua iliyosababisha kuagiza mkandarasi pamoja na mshauri
wake kuwekwa ndani kwa kushindwa kutekeleza maagizo ya serikali.
Uwanja wa Ndege Wafikia Asilimia 95
Wakati miradi ya barabara na stendi
ikiendelea kukumbwa na changamoto, ujenzi wa uwanja wa ndege wa Shinyanga
umefikia asilimia 95.
Mhandisi wa mradi huo, Ruburi Kahatano, alisema kazi
zilizobaki ni ukamilishaji wa jengo la abiria na majaribio ya vifaa kwa ajili
ya kutua ndege nyakati za usiku.
Mradi huo ulisainiwa mwaka 2017 na kuanza kutekelezwa mwaka 2023 kwa gharama ya Sh. 52 bilioni. Uwanja huo una urefu wa kilomita 2.2 na upana wa mita 30, ukiwa na uwezo wa kupokea ndege aina ya Bombardier Dash 8 Q400. Uwanja huo unatarajiwa kuwa msaidizi (Feeder Airport) kwa viwanja vikubwa kama Mwanza na Dar es Salaam.











0 Maoni