Mkurugenzi wa Elimu Msingi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Abdul Maulid.
Na Mwandishi Wetu,
Dodoma. Serikali imebaini kuwapo kwa udhaifu mkubwa wa stadi za kuhesabu miongoni mwa wanafunzi wa darasa la awali hadi la tatu, baada ya kufanya tathmini ya kitaifa ya Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK), matokeo hayo yameibua mjadala mpana kuhusu ubora wa msingi wa elimu ya hisabati katika ngazi za chini za shule za msingi.
Akizungumza Februari 25, 2026 katika kikao cha wadau wa elimu kilichoandaliwa na Shirika lisilo la kiserikali Chidren in Crossfire (CiC) jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Elimu Msingi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Abdul Maulid amesema kuwa, idadi kubwa ya wanafunzi katika ngazi za awali wanashindwa kufanya hesabu rahisi za kujumlisha na kutoa, huku wengine wakipata ugumu hata wa kutambua namba kwa usahihi,
“Msingi wa elimu ya mtoto unaanzia hapa, akishindwa kuhesabu mapema, anakuwa katika hatari ya kuendelea kufanya vibaya katika masomo mengine” amesema Maulid.
Ofisa Elimu mkoa wa Dodoma Kiduma Mageni ameeleza kuwa, “Tunapaswa kuangalia upya mbinu za ufundishaji katika ngazi ya awali, watoto wanahitaji kujifunza kwa vitendo zaidi kuliko nadharia pekee” Kauli hiyo inaonyesha umuhimu wa kubadili mbinu za ufundishaji ili ziendane na mahitaji ya watoto wadogo.
Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali Chidren in Crossfire (CiC) Craig Ferlaakizungumza katika kikao na wadau wa Elimu jijini Dodoma.
Wadau wa elimu wameeleza kuwa changamoto hiyo inaweza kusababishwa na mchanganyiko wa mambo, ikiwamo uhaba wa vifaa vya kufundishia, idadi kubwa ya wanafunzi darasani na uelewa mdogo wa mbinu shirikishi za kufundisha hesabu,
“Bila kuwa na mazingira rafiki ya kujifunzia, ni vigumu kwa mtoto kuelewa dhana za msingi za namba,” amesema mtaalamu mmoja wa elimu ya awali.
Aidha, Maulid ameonya kuwa udhaifu huo unaweza kuwa na athari za muda mrefu kwa maendeleo ya mwanafunzi kitaaluma, hasa katika masomo ya sayansi na teknolojia yanayohitaji uelewa mzuri wa hisabati, wataalamu wanasema hatua za haraka zinahitajika kuzuia pengo hilo kuendelea kupanuka kadri wanafunzi wanavyopanda madarasa.
Katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali imeahidi kuimarisha mafunzo kwa walimu wa darasa la awali na la chini pamoja na kuboresha mtaala ili uwe rafiki zaidi kwa ujifunzaji wa hesabu,
“Tutahakikisha walimu wanapatiwa mafunzo ya mara kwa mara na vifaa vya kufundishia vinavyokidhi mahitaji,” imeeleza taarifa ya wizara husika.
Wazazi nao wametakiwa kushirikiana na walimu kwa kuwasaidia watoto kufanya mazoezi ya hesabu nyumbani ili kuimarisha kile wanachojifunza shuleni, wadau wanaamini kuwa kwa ushirikiano wa pamoja kati ya serikali, walimu na wazazi, kiwango cha uelewa wa kuhesabu kwa wanafunzi wa awali kinaweza kuongezeka na kuweka msingi imara wa elimu yao ya baadaye.

.jpeg)

.jpeg)

0 Maoni