RATIBA YA MAZISHI YA KARDINALI PENGO

 

Dar es Salaam. Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam limetangaza rasmi ratiba ya mazishi ya Kardinali Polycarp Pengo ambaye ni Askofu Mkuu mstaafu wa jimbo hilo, aliyefariki dunia Februari 19, 2026 baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Taarifa za Kanisa zinaeleza kuwa kiongozi huyo wa kiroho alifariki akiwa anapatiwa matibabu katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete Cardiac Institute jijini Dar es Salaam, na kuacha simanzi kwa waumini na watanzania kwa ujumla.


Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, mwili wa marehemu utaanza kuagwa rasmi leo Ijumaa Februari 27, 2026 katika Kanisa Kuu la St Joseph’s Cathedral, ambako utawekwa ili kutoa nafasi kwa waumini na wananchi kutoa heshima zao za mwisho.


Waombolezaji wanatarajiwa kufika kanisani hapo kuanzia asubuhi hadi jioni, wakishiriki sala na ibada maalum zitakazoandaliwa kwa ajili ya kumuombea marehemu apumzike kwa amani ya milele.


Aidha, Misa Takatifu ya kumuombea marehemu itaadhimishwa jioni ya leo Ijumaa, Februari 27, 2026 ikiongozwa na viongozi wa Kanisa, sambamba na kuendelea kwa maombi na tafakari za waumini.


Siku ya kesho Jumamosi Februari 28, 2026 ibada kuu ya Misa ya Mazishi itafanyika asubuhi katika kanisa hilo hilo, kabla ya mwili wa Kardinali Pengo kuondolewa kwa ajili ya maziko rasmi.


Baada ya ibada hiyo, mwili utapelekwa katika Kituo cha Hija cha Pugu Pilgrimage Centre kwa ajili ya mazishi, eneo alilolichagua mwenyewe kama mahali pa mapumziko yake ya mwisho.


Viongozi wa Serikali, dini mbalimbali na mamia ya waumini kutoka ndani na nje ya nchi wanatarajiwa kushiriki katika mazishi hayo, wakitambua mchango mkubwa wa Kardinali Pengo katika uongozi wa Kanisa na maendeleo ya jamii nchini.

Chapisha Maoni

0 Maoni