MRADI WA UMEME JUA KISHAPU, WATOA MWANGA ZANZIBAR

Mwenyekiti wa kamati ya kudumu ya hesabu za serikali la baraza la wawakilishi Zanzibar (PAC) Kombo Mwinyi Shehe akizungumza katika ziara, mradi wa umeme jua uliopo wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Na Mwandishi Wetu, Shinyanga.

Kishapu. Wakati Zanzibar ikiendelea kukabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme, matumaini mapya yanaonekana kuibuka kufuatia ziara ya Kamati ya Kudumu ya Hesabu za Serikali (PAC) ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar katika mradi wa umeme jua unaotekelezwa wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.

Ziara hiyo imelenga kujifunza kwa kina namna mradi huo ulivyotekelezwa kwa kuzingatia masuala ya kijamii na mazingira, ili uzoefu huo uweze kutumika kama sehemu ya suluhisho la muda mrefu kwa tatizo la umeme visiwani Zanzibar.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo Aprili 2, 2026, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Mwinyi Shehe, alieleza wazi kuwa mahitaji ya umeme Zanzibar yamekuwa yakiongezeka kwa kasi huku kiwango kilichopo kikishindwa kukidhi mahitaji hayo. Kutokana na hali hiyo, aliitaka TANESCO kuongeza kiwango cha umeme kinachouzwa Zanzibar ili kukabiliana na uhaba huo.

Katika hatua nyingine, wajumbe wa kamati hiyo walionesha dhamira ya kutaka kujifunza zaidi kuhusu namna miradi ya nishati jadidifu inavyoweza kuendeshwa bila kuathiri mazingira. Mwenyekiti wa Kamati ya Mazingira Zanzibar, Mhe. Mohammed Manzi Haji, alisisitiza umuhimu wa kufuata taratibu sahihi za uhifadhi wa mazingira, akibainisha kuwa maarifa watakayoyapata yatawasaidia kupanga na kutekeleza miradi kwa ufanisi zaidi Zanzibar.

Kwa upande wake, mjumbe Salma Mussa Bilal aliibua hoja ya upanuzi wa miradi kama hiyo katika maeneo mengine yenye rasilimali ya jua, akitaka kujua mikakati ya kuhakikisha uzalishaji wa umeme unaongezeka kupitia nishati jadidifu ili kukidhi mahitaji ya wananchi.

Akijibu hoja hizo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Timothy Mgaya, alieleza kuwa serikali inaendelea na juhudi mbalimbali za kuboresha upatikanaji wa umeme Zanzibar, ikiwemo utekelezaji wa mradi wa kebo ya chini ya bahari unaounganisha visiwa vya Unguja na Mafia, ambao unatarajiwa kuongeza kiwango cha umeme kinachopatikana.

Aidha, Mgaya alibainisha kuwa miradi ya umeme jua inaendelea pia katika maeneo mbalimbali nchini kama Dodoma, Manyara na Same kupitia uwekezaji wa sekta binafsi, akisisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuongeza uzalishaji wa umeme nchini.

Katika kuhakikisha maendeleo haya hayaji kwa gharama ya mazingira, TANESCO imeendelea kusisitiza uzingatiaji wa taratibu zote za uhifadhi wa mazingira, ikiwemo kupata vibali kutoka NEMC. Katika mradi wa Kishapu, hatua maalum zilichukuliwa kulinda mfumo wa ikolojia kwa kuepuka ujenzi wa ukuta mkubwa na badala yake kuweka uzio wa kawaida unaoruhusu viumbe hai kuendelea kuishi katika mazingira yao.

Kwa ujumla, ziara hiyo imeonesha mwelekeo mpya wa Zanzibar katika kutafuta suluhisho mbadala la umeme kupitia miradi ya nishati jadidifu, huku ikitoa msisitizo mkubwa katika kulinda mazingira na kushirikisha wadau mbalimbali wa maendeleo.

Chapisha Maoni

0 Maoni