MRADI WA UMEME JUA WAFIKIA ASILIMIA 95.5, KUKUZA UCHUMI KANDA YA ZIWA

 

Shinyanga. Mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa jua unaotekelezwa mkoani Shinyanga umefikia hatua ya asilimia 95.5 ya utekelezaji katika awamu ya kwanza, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa umeme na kusaidia kukuza shughuli za kiuchumi katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Akizungumza Machi 13, 2026 wakati wa ziara ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Lazaro Twange, amesema kuwa mradi huo tayari umeanza kuonesha mafanikio makubwa baada ya kuunganishwa kwenye gridi ya taifa wiki mbili zilizopita.

Twange ameeleza kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo inazalisha megawatt 50 za umeme, ambao utaongeza uwezo wa usambazaji wa umeme katika maeneo mbalimbali ikiwemo kituo cha kupooza umeme cha mkoa wa Simiyu, amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza changamoto za umeme katika mikoa ya Kanda ya Ziwa.


“Awamu ya kwanza ya mradi huu inazalisha megawatt 50 na tayari umefikia asilimia 95.5 ya utekelezaji, wiki mbili zilizopita uliunganishwa katika gridi ya taifa na uzalishaji huu utasaidia shughuli mbalimbali za kiuchumi” amesema Twange.

 

Ameongeza kuwa umeme huo utachochea maendeleo katika sekta muhimu za uchumi kama uchimbaji wa madini, viwanda vya kuchakata pamba, pamoja na kusaidia miundombinu ya usafiri wa reli ya kisasa (SGR) ambayo ni sehemu ya miradi mikubwa ya maendeleo nchini.


Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, Subira Mgalu, amesema kamati hiyo imeridhishwa na maendeleo ya mradi huo pamoja na matumizi ya fedha za utekelezaji.


Amesema kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo imegharimu takribani Shilingi bilioni 118, na tathmini ya kamati inaonesha kuwa fedha hizo zimetumika kwa ufanisi kulingana na kazi iliyotekelezwa.


“Tunawapongeza wakandarasi na wote waliohusika na utekelezaji wa mradi huu, tumejiridhisha kuwa thamani ya fedha zilizotolewa inaendana na hatua ya utekelezaji wa mradi hadi kufikia kuunganishwa kwenye gridi ya taifa” amesema Mgalu.

Naye Meneja wa Mradi wa Umeme wa Jua, Emmanuel Anderson, amesema mradi huo unatumia zaidi ya paneli 82,000 za sola, ambazo zina uwezo wa kudumu kwa kipindi kisichopungua miaka 25 tangu kuanza kutumika.


Ameeleza kuwa paneli hizo ndizo zinazowezesha uzalishaji wa megawatt 50 katika awamu ya kwanza ya mradi huo.


Aidha, Anderson amesema maandalizi ya awamu ya pili ya mradi, ambayo inalenga kuzalisha megawatt 100, yanaendelea na yanatarajiwa kuanza hivi karibuni ili kukamilisha mradi mzima wa umeme wa jua mkoani Shinyanga.


Mradi huo wa umeme wa jua ni sehemu ya juhudi za Serikali kuongeza matumizi ya nishati safi na endelevu, huku ukisaidia kuimarisha upatikanaji wa umeme kwa shughuli za maendeleo, viwanda na huduma za kijamii katika maeneo mbalimbali nchini.


Kwa kukamilika kwake, mradi huu unatarajiwa kuwa moja ya miradi muhimu itakayochochea ukuaji wa uchumi katika Kanda ya Ziwa na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa umeme kwa wananchi na wawekezaji.

Chapisha Maoni

0 Maoni