Dar es Salaam. Tanzania imepata pigo kufuatia kifo cha Waziri wa zamani na mwanasiasa mkongwe, William Lukuvi, aliyefariki dunia ghafla kutokana na mshituko wa moyo.
Taarifa za awali zinaeleza kuwa Lukuvi alipata tatizo hilo la ghafla la kiafya lililosababisha kifo chake, jambo lililozua mshtuko mkubwa kwa viongozi wa serikali, familia, marafiki na wananchi kwa ujumla.
Kifo chake kimethibitishwa na vyanzo vya karibu na familia pamoja na viongozi wa serikali, waliobainisha kuwa mwanasiasa huyo alikuwa akiendelea na majukumu yake ya kawaida kabla ya umauti kumkuta.
Lukuvi alijizolea umaarufu mkubwa katika siasa za Tanzania, akihudumu katika nyadhifa mbalimbali za uongozi, ikiwemo uwaziri katika sekta ya ardhi na baadaye Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu). Alijulikana kwa msimamo wake mkali katika kushughulikia masuala ya ardhi na kupambana na migogoro iliyokuwa ikiikumba sekta hiyo.
Katika kipindi cha uongozi wake, alisifiwa na baadhi ya wananchi kwa uthubutu wake, huku wengine wakimkosoa kutokana na maamuzi yake ya moja kwa moja dhidi ya watendaji waliokiuka sheria.
Viongozi mbalimbali wa kitaifa wameanza kutuma salamu za rambirambi wakieleza masikitiko yao juu ya kifo hicho, wakimtaja Lukuvi kuwa kiongozi aliyekuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi.
Mpaka sasa, taratibu za mazishi zinatarajiwa kutangazwa na familia kwa kushirikiana na serikali.
Kifo cha Lukuvi kinaacha pengo kubwa katika uongozi na siasa za Tanzania, ambapo anakumbukwa kama mmoja wa viongozi waliokuwa na msimamo thabiti katika utendaji wa kazi za umma.


0 Maoni