BILIONI 22.3 KUBORESHA SEKTA YA AFYA, SHINYANGA.

Na Mwandishi Wetu,

 Shinyanga. Mshauri elekezi wa mradi kutoka kampuni ya Volumetric Arch Consult Berno Batenamani ameeleza kuwa, mradi wa ujenzi wa jengo la mama na mtoto lenye ghorofa tano pamoja na maabara utaanza baada ya wiki mbili kuanzia leo, ambapo itakuwa Juni 19, 2026 na utatekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili,

Akizungumza leo Juni 05, 2026 katika hafla fupi ya makabidhiano ya eneo la ujenzi katika Hospitali ya rufaa ya mkoa ya Shinyanga (Mwawaza) Batenamani ameeleza kuwa, mradi huo utagharimu kias cha Sh. 22.3 bilioni hadi kukamilika kwake na utakuwa na majengo mawili,

“Ujenzi huo unatarajiwa kuanza Juni 19, 2026 na kukamilika Juni 18, 2028 ambapo utachukua kipindi cha miaka miwili, na hadi kukamilika kwake utagharimu kiasi cha zaidi ya Sh. 22.3 bilioni” amesema Batenamani.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mkurugenzi idara ya tiba Wizara ya afya kutoka Dodoma Daktari Festo Mapunda amemtaka mhandisi kuwapa nafasi za vibarua kwa wananchi wa Shinyanga ili waweze kunufaika na ujenzi wa mradi huo,

“Itapendeza kama mhandisi utawapa nafasi za vibarua wananchi wazawa ambao ni wa eneo husika, ili na wao waweze kunufaika na ujenzi wa mradi huu kwa kipindi ambacho unatekelezwa” amesema Mapunda.

Naye mtekelezaji wa mradi huo ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji kutoka kampuni ya Amar Builders Limited Vipul Naran amesema kuwa watafanya kazi kwa uaminifu na kwa kushirikiana na uongozi wa serikali ya mkoa na kumaliza ndani ya mkataba,


“Tutashirikiana bega kwa bega na serikali katika utekelezaji wa mradi huu, pia tutahakikisha tunajenga kama ramani inavyosema na kumaliza ndani ya wakati, huku tukiwapa vipaumbele vya ajira za vibarua wananchi wa eneo hili” amesema Naran.


Mbali na hilo, mwakilishi kutoka Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga Mhandisi Johanes Byabato amesema kuwa kuwa ujenzi wa jengo la mama na mtoto mkoani Shinyanga, unalenga kuboresha utoaji wa huduma kwa mama na mtoto na sekta ya afya kwa mkoa wa Shinyanga.

Aidha, Mganga mfawidhi kutoka Hospitali ya rufaa ya mkoa wa Shinyanga (Mwawaza) Daktari John Luzila ametoa shukrani kwa serikali kufikia hatua ya utekelezaji wa mradi huo ambao utahudumia wanawake 66 pamoja na watoto 96,

“Naishukuru serikali kwa utekelezaji wa mradi huu, ambao utahusisha jengo la mama na mtoto na maabara ya kisasa na kuongeza ufanisi wa utendaji kazi, pia katika majengo haya ghorofa ya 3 na 4 itakuwa kwa ajili ya watoto wachanga, vyumba vya chini vitakuwa kwa ajili ya wanawake wanaotaka kujifungua na pia kutakuwa na vitanda saba vya vyumba binafsi” amesema Dkt. Luzila.

Pia ameongeza kuwa, “Katika eneo la chini kutakuwa na vyumba viwili vya upasuaji na kutakuwa na vitanda 11 kwa wagonjwa wa kulazwa na 7 wa kujifungua” ameongeza Dkt. Luzila.

Chapisha Maoni

0 Maoni