Na Mwandishi Wetu,
Kishapu. Kamanda wa jeshi la polisi mkoani Shinyanga Janeth Magomi amethibitisha kuwashikilia watu 75 waliohusika katika matukio mawili ya kusababisha vurugu katika kijiji cha Sanjo kata ya Idukilo wilayani Kishapu,
“Jeshi la polisi limekamata watuhumiwa 75 waliohusika katika matukio mawili tofauti, tukio la kwanza lilitokea Mei 28, 2026 katika kijiji cha Sanjo kata ya Idukilo wilaya ya Kishapu, mkoani Shinyanga, ambapo mtendaji wa kata ya Idukilo aitwae Masembe Msele (50) akiwa na Ofisa maendeleo wa kata ya Mwadui Luhumbo aitwaye Rose Shayo (38) mwenyekiti wa kijiji cha Sanjo pamoja na wajumbe watatu wa serikali ya kijiji wakiwa katika zoezi la kuingiza kaya maskini katika mfumo wa TASAF walivamiwa na watu waliokuwa kwenye pikipiki mbili” amesema Magomi.
Pia ameongeza kuwa, “Watu hao walianza kuwapiga na kuwanyang’anya nyaraka hizo zilizokuwa na baadhi ya majina na kuondoka wakidai hawataki kuona kiongozi yoyote wa serikali akifanya kazi ndani ya kata ya Idukilo, ambapo vurugu hizo zilisababishwa na wananchi kumkataa diwani wa kata hiyo, ambaye alikimbia eneo hilo” ameongeza.
“Tukio la pili lilitokea Juni 01, 2026 saa sita na nusu usiku katika kata hiyo ambapo, kuna baadhi ya wanakijiji walipigwa kwa madai kuwa ndio wanatoa siri kwa polisi na kwa mkuu wa Wilaya kwa kupeleka majina ya wanaofanya fujo” amesema.
Magomi ameongeza kuwa, “Katika vurugu hizo walifanya uharibifu wa pikipiki na kuvunja baadhi ya maduka ya wafanyabiashara ambapo jeshi lapolisi lilifika na kuwakamata waharifu hao” amesema Magomi.
Hata hivyo Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linakemea vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na baadhi ya wananchi wa kata hiyo ya Idukilo na halitasita kuwachukulia hatua za kisheria ambao wataendelea kujihusisha na vitendo hivyo.


0 Maoni