WAZAZI WATAJWA KUWA CHANZO CHA UTORO KWA WANAFUNZI SHULENI

 

Na Mwandishi Wetu,

Kishapu. Vitendo vya baadhi ya wazazi kuwaachisha watoto shule katika shule ya msingi Mwagembe iliyopo kata ya Mwataga, Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, vimetajwa kuwa chanzo kikubwa cha wanafunzi wengi kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari na kunyimwa haki yao ya msingi ya kupata elimu.


Hayo yamebainishwa katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Mwagembe kwa lengo la kutoa elimu kuhusu huduma za msaada wa kisheria kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid.

Wakazi wa kijiji hicho akiwemo Agrey Godson wamesema bado kuna wazazi wanaowalazimisha watoto wao kufanya vibaya katika masomo ili wasiingie sekondari, huku wengine wakiwazuia kabisa kuendelea na elimu kutokana na sababu mbalimbali za kifamilia na kiuchumi.


Kwa mujibu wa wananchi hao, hali hiyo imekuwa ikiwakatisha tamaa wanafunzi wanaopenda kusoma na kusababisha baadhi yao kuona elimu haina umuhimu katika maisha yao.


Kwa upande wake, Ofisa ustawi wa jamii wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, Mwajuma Abeid, amesema matukio ya ukatili dhidi ya watoto na wanawake bado ni changamoto kubwa katika wilaya hiyo.

 

Amesema ofisi yake inapokea kesi mbalimbali zinazohusiana na ukatili ikiwemo ulawiti na ubakaji, huku akieleza kuwa kampeni hiyo inalenga kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kupinga vitendo hivyo kwa kutoa taarifa mapema na kutowaficha wahusika.

Chapisha Maoni

0 Maoni