Na Mwandishi Wetu,
Shinyanga. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita ametoa wito kwa wazazi na wananchi kushirikiana na walimu pamoja na viongozi wa maeneo yao katika kulinda miundombinu ya shule, kufuatia matukio ya wizi wa milango na madirisha yanayoharibu mazingira ya kujifunzia wanafunzi.
Mhita ametoa kauli
hiyo leo Mei 15, 2026 wakati wa uzinduzi wa shule mpya ya awali na msingi Tinde
‘B’ iliyopo kijiji cha Nyambui, kata ya Tinde katika Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga.
Amesema baadhi ya
wananchi wamekuwa wakifumbia macho vitendo vya vijana wanaoharibu mali za
shule, hali ambayo inachangia kudhoofisha usalama na mazingira bora ya elimu.
“Wazazi tuwe na
uchungu na vitu vyetu. Kuna wengine wanajua kabisa mtoto au kijana wa mtu
ameshiriki kuiba miundombinu ya shule lakini wanakaa kimya. Hii inaharibu
mazingira ya wanafunzi wanaosoma hapo,” amesema Mhita.
Mbali na suala la
usalama wa shule, Mhita amesema serikali ipo kwenye mpango wa kupanua eneo la
shule hiyo ili kupata nafasi ya uwanja wa michezo kwa ajili ya kukuza vipaji
vya wanafunzi.
Amesema michezo ni
sehemu muhimu ya maendeleo ya watoto na itasaidia wanafunzi kupata nafasi ya
kuonyesha vipaji vyao wakiwa shuleni.
Katika hatua ya kuunga mkono jitihada hizo, Mbunge wa Jimbo la Itwangi, Azza Hillal ametoa vifaa vya michezo kwa shule za Tinde ‘A’ na Tinde ‘B’, ikiwemo jezi na mipira kwa wanafunzi wa kike na wa kiume.
Azza amesema msaada
huo unalenga kuhamasisha wanafunzi kushiriki michezo sambamba na masomo yao.
“Tumetoa dazani
nane za nguo za michezo pamoja na mipira minne kwa shule hizi mbili ili
kusaidia kukuza vipaji vya wanafunzi wetu,” amesema Azza.
Kwa upande wake mwenyekiti wa Halmashuri ya
wilaya ya Shinyanga Seth Msangwa ametoa shukrani kwa mbunge wa jimbo la Itwangi
Azzah Hillal pamoja na serikali ya Rais dr. Samia Suluhu Hassan kwa ujenzi wa
shule hiyo ambayo imegharimu zaidi ya Sh 340 milioni.



0 Maoni